Azimio kuhusu kusimamia madeni na kupambana na rushwa katika Afrika


African Union

Azimio kuhusu kusimamia madeni na kupambana na rushwa katika Afrika

BUNGE LA AFRIKA,LIKIZINGATIA Ibara ya 17 ya Mkataba Anzilishi wa Umoja wa Afrika ulioanzisha Bunge la Afrika ili kuhakikisha ushiriki kamili wa watu wa Afrika katika maendeleo na ushirikiano wa kiuchumi wa bara;LIKIZINGATIA pia Ibara ya 3 ya Protokali ya Mkataba Ulioanzisha Jumuiya ya Uchumi ya Kanda inayohusiana na Bunge la Afrika, na Kanuni ya 4 (a) ya Kanuni za Uendeshaji wa Bunge la Afrika, inayolipa BA mamlaka ya kuwezesha utekelezaji wa sera, malengo na programu za Umoja wa Afrika na kusimamia utekelezaji wake mzuri;LIKIREJEA Azimio Maalum la Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa UA kuhusu Usafirishaji Haramu wa Fedha kwenye Mkutano wa Kawaida wa Ishirini na Nne huko Addis Ababa, Ethiopia, mwezi Januari 2015 na Mapendekezo ya Ripoti ya Jopo la Viongozi kuhusu Usafirishaji Haramu wa Fedha kutoka Afrika;LIKIREJEA PIA Azimio la Kushinda Mapambano dhidi ya Rushwa: Njia Endelevu katika Mageuzi ya Afrika lililopitishwa na Bunge la Afrika tarehe 17 Mei 2017;LIKISIKITISHWA na ukweli kwamba rushwa na usafirishaji haramu wa fedha vinatishia malengo yetu ya kukomesha umaskini na njaa katika Afrika na kufikia maendeleo endelevu katika vipengele vyake vitatu kupitia kuhimiza ukuaji jumuishi wa uchumi, kulinda mazingira na kuhimiza kuthamini makundi yote ya jamii, ahadi thabiti za kisiasa za kushughulikia changamoto zinazoletwa na rushwa na usafirishaji haramu wa fedha nje ya Afrika lazima kuongezwe;LIKISIKITISHWA PIA kwamba usafirishaji haramu wa fedha unasababisha uhaba wa fedha zilizopo kwa Serikali kutumia katika maendeleo ya taifa, ambako kunasababisha ukopaji na kuongeza viwango vya madeni ya serikali kuu katika Afrika;LIKISIKITISHWA ZAIDI kwamba ununuzi duni wa umma, kutokuwepo kwa uwazi na usimamizi mbaya wa kodi unaofanywa na Serikali umesababisha mapato kidogo na kuhitaji kukopa;LIKITAMBUA KWA MASIKITIKO kwamba motisha na kutokuwa na ukomo katika kodi bila ya kupata kwanza idhini ya Bunge na ukosefu wa ufuatiliaji na tathmini katika hilo kunaziweka nchi katika hatari ya kupoteza mapato na kuongezeka uwezekano wao wa kuingia katika mikataba ya kulipa madeni;LIKITAMBUA PIA jukumu muhimu la Kamati ya Ukaguzi na Hesabu za Umma katika kuyasaidia Mabunge kuzuia rushwa na IFFs, na katika kudhibiti madeni;LIKITAMBUA ZAIDI kwamba Mabunge yanaweza kutumia madaraka yake ya usimamizi katika mzunguko wa bajeti, uwajibikaji kwa matumizi ya fedha za umma na uwakilishi wa watu wa kuziwajibisha serikali kwa kulipa fedha za umma kama ilivyoamuliwa katika mpango wa bajeti, ikiwa ni pamoja na makubaliano katika deni la umma;LIKIZINGATIA Azimio la Kampala la Kamati za Muungano wa Afrika wa Hesabu za Umma (AFROPAC) lililopitishwa tarehe 22 Novemba 2018;LIKITHAMINI uwasilishaji wa kitaalamu uliofanywa na wawakilishi wa Muungano wa Taasisi za Ukaguzi za Nchi Zinazozungumza Kiingereza Afrika (AFROSAI-e), AFROPAC, Mtandao wa Wabunge wa Afrika wa Kupambana na Rushwa (APNAC), Shirika la Fedha Duniani (IMF), Jukwaa la Usimamizi wa Kodi Afrika (ATAF) na Bodi ya Kupambana na Rushwa ya Umoja wa Afrika (AU-ABC);LIKIDHAMIRIA kuwezesha utekelezaji wa uamuzi wa UA wa kutokomeza rushwa na kuhimiza utamaduni wa uwazi na utawala bora kulingana na hati za kisheria na kisera zinazohusika za UA;LINASHAWISHIKA kwamba kuanzishwa kwa muungano ndani ya Bunge la Afrika wa kusimamia madeni na kukomesha rushwa kutawapa Wabunge wa BA muundo na jukwaa linalofaa la kushughulikia kwa uendelevu na kuliweka suala la usimamizi wa madeni na ukomeshaji wa rushwa katika ya ajenda za juu za kisiasa na kisheria kwenye ngazi za taifa na bara;KWA MUJIBU WA Kanuni ya 5 (b), (c) na (d) ya Kanuni za Uendeshaji wa Bunge la Afrika, ambayo, pamoja na mambo mengine, inalipa BA mamlaka ya kuandaa mjadala, kujadili, kutoa maoni, kutoa mapendekezo na kuchukua maazimio kuhusu malengo na masuala yoyote yanayohusiana na Umoja wa Afrika na vyombo vyake, Jumuiya za Uchumi za Kanda, Nchi Wanachama na vyombo na taasisi zao;
SASA LINAAZIMIA:
1.KUHIMIZA uridhiaji kwa wote, utumikaji katika nchi na utekelezaji wa mikataba ifuatayo ya Umoja wa Afrika inayohusiana na kupambana na rushwa:
i.Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia & Kupambana na Rushwa;
ii.Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia & Kupambana na Rushwa;
iii.Mkataba wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala;
iv.Protokali ya Mkataba Uliyoanzisha Umoja wa Afrika unaohusiana na Bunge la Afrika;
v.Protokali ya Marekebisho ya Mkataba wa Sheria za Mahakama ya Afrika na haki za Binadamu;
2.KUJIHUSUSHA na Mabunge ya Afrika ya Taifa na Kanda kwa ajili ya kutumia kikamilifu madaraka yake ya kutunga sheria katika kutunga au kurekebisha sera na sheria za taifa zinazohusiana na mapambano dhidi ya rushwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hakuna ufilisi wa mali bila ya kushtakiwa na kwamba sheria ya uhalifu inahamisha wajibu wa kuthibitisha kutoka kwa mwendesha mashtaka kwenda kwa mtuhumiwa kwa suala la rushwa na IFFs;
3.PIA KUJIHUSISHA na Mabunge ya Taifa na Kanda ya Afrika kwa ajili ya utekelezaji mzuri wa jukumu lao la usimamizi, utungaji sheria na uwakilishi ili kuhakikisha usimamizi unaofaa wa madeni ya serikali na kuvunja mzunguko wa rushwa, hususan kupitia ufuatiliaji kwa wakati na usimamizi wa ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi na ukaguzi wa deni la serikali, mtiririko wa fedha, mapato na ununuzi.
4.KUTETEA kwa pamoja na Vyombo vya Sera vya UA kwa ajili ya uanzishaji au uimarishaji, pale inapofaa, wa taratibu na mikakati ya taifa na bara inayolenga katika usimamizi na upunguzaji unaofaa wa madeni katika Afrika, ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji, uwazi na ushiriki wa raia katika michakato inayoongoza katika kuweka mikataba ya madeni ya serikali;
5.KUTETEA kwa pamoja na Vyombo vya Sera vya UA na Nchi Wanachama kwa ajili ya kuimarisha madaraka, uhuru na kuwa na uwezo kwa taasisi zote za taifa na bara zenye madaraka yanayohusika ya kupambana na rushwa, hususan Kamati ya Ukaguzi na Hesabu za Umma, taasisi za Kupambana na Rushwa, taasisi za ukaguzi wa hesabu na mfumo wa sheria;
6.KUSAIDIA na KUHIMIZA wajinu wa mitandao ya Mabunge ya kupambana na rushwa, raia, vyombo vya habari na asasi za kiraia katika kuendeleza utamaduni wa uwazi, uadilifu na uwajibikaji, na katika kuzuoa uhamishaji haramu wa fedha na madeni yasiyolipika;
7.KUFANYA KAZI na wabia wenye nia katika uoanishaji wa sheria na viwango vya taifa katika uwanja wa usimamizi wa madeni na mapambano dhidi ya rushwa, pamoja na kupitia uandaaji, upitishaji na ulinganishaji wa sheria za mfano za bara, makubaliano ya mfano ya utozaji kodi mara mbili na viwango vingine vya kisekta kwa ajili ya kutumika, kurekebishwa au kupitishwa na Nchi Wanachama wa UA;
8.Kwa mtazamo wa ushughulikiaji endelevu na kuliweka suala la usimamizi wa madeni na rushwa katika ajenda za juu za siasa na sheria za Afrika, LINAANZISHA Muungano wa Bunge la Afrika wa Kusimamia Madeni na Kupambana na Rushwa (PAPA-DMAC), ambao utaandaliwa na kusimamiwa kama ifuatavyo:
(i)Wajumbe wote wa Kamati ya Fedha, Kamati ya Ukaguzi na Hesabu za Umma na Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu watakuwa wajumbe wa PAPA-DMAC, ili mradi kwamba Mbunge yeyote wa BA anayependelea kushughulikia usimamizi wa madeni na kupambana na rushwa katika Afrika anaweza kushiriki katika shughuli za PAPA-DMAC.
(ii)PAPA-DMAC utakuwa na Kamati ya Utendaji, ambayo itaundwa na Weenyeviti wa Kamati ambazo zimetajwa katika Kifungu cha 7.1 na watakuwa chini ya usimamizi wa Uongozi wa BA.
(iii)Muundo na ufanyajikazi wa PAPA-DMAC utarekebishwa kulingana na vifungu vinavyohusika ambavyo vinatumika kwa Kamati za Kudumu zote za Bunge la Afrika.
9.KUTOA SHUKRANI kwa AFROPAC, AFROSAI, APNAC, ATAF, AU-ABC na IMF kwa kuendelea kusaidia na kutoa msaada wa kitaalamu kwa BA na KUELEZA nia yao ya kurasimisha na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati uliopo na unaotarajiwa ili kuongeza msaada wa kitaalamu na kifedha kwa shughuli zake zinazohusiana na kukomesha mzunguko wa rushwa katika Afrika.
Midrand, Afrika Kusini17 Oktoba 2019
▲ To the top