Pendekezo kuhusu wajibu wa kijamii wa Wabunge katika mapambano dhidi ya ajira kwa watoto walio katika maeneo ya migodi


African Union

Pendekezo kuhusu wajibu wa kijamii wa Wabunge katika mapambano dhidi ya ajira kwa watoto walio katika maeneo ya migodi

BUNGE LA AFRIKA,LIKIZINGATIA Ibara ya 17 (1) ya Mkataba Ulioanzisha Umoja wa Afrika ambao ulianzisha Bunge la Afrika ili kuhakikisha ushiriki kamili wa watu wa Afrika katika maendeleo na ushirikiano wa kiuchumi wa bara;LIKIZINGATIA PIA Ibara ya 3 ya Protokali ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Uchumi ya Kanda inayohusiana na Bunge la Afrika na ibara ya 4 (a) ya Kanuni za Undeshaji wa Bunge la Afrika;LIKIZINGATIA PIA, vifungu vya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Mtoto na Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto, ambapo nchi nyingi za Afrika zimeridhia na kuingiza katika sheria zao, hususani kwa kupiga marufuku ajira kwa watoto;LIKIZINGATIA mahitimisho ya Ripoti ya ziara ya kutafuta ukweli wa mambo kuhusu wajibu wa wabunge katika mapambano dhidi ya ajira kwa watoto katika maeneo ya migodi, iliyofanywa na Kamati ya Afya, Kazi na Masuala ya Kijamii, kuanzia tarehe 16 hadi 18 Septemba, 2019 huko Abidjan, Ivory Coast;LIKITAMBUA PIA kwamba Sekta ya madini ni moja ya sekta muhimu zaidi barani Afrika, lakini iko kwenye orodha ya shughuli hatari zaidi ulimwenguni, hususani kwa watoto;LIKISIKITISHWA na unyonyaji wa watoto katika shughuli za kiuchumi ambazo huwasababishia unyanyasaji wa aina mbalimbali na hatari kubwa ya kudhoofika kwa afya na ukuaji wao;LIKISIKITISHWA ZAIDI na takwimu kubwa zinazooneshwa na utafiti wa UNICEF wa mwaka 2016 ambapo zinaonesha kwamba huko Ivory Coast, kazi hatarishi zinaathiri watoto 1,622,140 kati ya 2,213,708 wanaofanya shughuli za kiuchumi, au sawa na asilimia 73.3 ya watoto.LIKITAMBUA kwamba sekta ya kilimo inaajiri watoto wengi zaidi takribani asilimia 56.2, sekta ya huduma asilimia 41.9, asilimia 21.5 ya watoto wenye umri wa miaka kati ya 5 na 7 nchini Ivory Coast wanafanya kazi hatarishi hususani uvunjaji na usafirishaji mawe, upasuaji wa miamba kwa kutumia baruti, kazi za chini ya ardhi, uchimbaji na usafishaji wa dhahabu kwa kutumia zebaki na cyanide;LIKIPONGEZA juhudi za Umoja wa Afrika za kuimarisha ulinzi wa haki za watoto kupitia uandaaji wa Mpango Kazi wa Miaka Kumi unaohusiana na kukomesha ajira kwa watoto, ajira za shuruti na utumwa mamboleo na usafirishaji haramu wa binadamu barani Afrika;LIKIPONGEZA PIA juhudi za Ivory Coast kwa kuimarisha sera zake za ajira kwa watoto, hususan kupitia Azimio la Mpango wa Pamoja wa mwaka 2010 lenye lengo la kusaidia utekelezaji wa Protokali ya Harkin-Engel; kusainiwa kwa Makubaliano ya Ushirikiano katika eneo la Afrika Magharibi pamoja na Ghana na Burkina Faso; uundaji wa kamati ya kitaifa inayohusisha wizara mbali mbali (CIM) na Kamati ya Usimamizi ya Kitaifa (CNS) pamoja na kupitishwa kwa sera za kitaifa, hususan mpango kazi wa 2019-2021 wa kupambana na ajira kwa watoto;LIKIRIDHISHWA na maandalizi yote yaliyofanywa na Ivory Coast kwa ajili ya kuwezesha ziara ya ujumbe wa BA na LIKIPONGEZA ushirikiano kati ya wabunge, wawakilishi wa wizara mbalimbali na asasi za kiraia za Ivory Coast ambao wameunga mkono juhudi za Wabunge wa Bunge la Afrika kwa kuwapa data na habari za kuaminika,LIKIKUMBUSHA kwamba nchi wanachama zina jukumu la kutoa hifadhi ya jamii kwa wananchi kwa kuweka mazingira wezeshi ili kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi kama elimu, maji, nyumba na huduma za afya;
SASA LINAAZIMIA:
1.Kwa nchi wanachama:
i.KUKUZA na KULINDA haki za binadamu, hususan zile za makundi yaliyo katika mazingira hatarishi kama watoto kupitia uimarishaji wa mifumo ya kitaifa ya kulinda haki hizi.
ii.KUUNDA au, ikibidi, KUFUFUA mabunge ya watoto kama jukwaa linalowawezesha kushughulikia na kutatua matatizo yao kwa njia nzuri;
2.Kwa Wabunge wa nchi wanachama KUTUMIA kikamilifu mamlaka yao ya kusimamia shughuli za serikali na KUPITISHA sheria husika na kuhakikisha zinatekelezwa kikamilifu huku kukiwa na adhabu dhidi ya wale wanaokiuka sheria hizo.
3.Kwa Kamati ya Afya, Kazi na Masuala ya Kijamii kufanya mashauriano ya kikanda kuhusu utumikishaji wa watoto kwa lengo la kuimarisha mafanikio yao kwenye ulinzi wa haki zao.
Limepitishwa Midrand, Afrika KusiniTarehe 17 Oktoba 2019
▲ To the top